China kuongeza uwekezaji katika miradi yenye utoaji mdogo wa kaboni barani Afrika
2022-01-26 14:25:49| CRI

China kuongeza uwekezaji katika miradi yenye utoaji mdogo wa kaboni barani Afrika_fororder_KDP3666_w1175.JPG

Mkurugenzi wa Ofisi ya Ushirikiano wa Kimataifa ya Idara ya Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi katika Wizara ya Ikolojia na Mazingira ya China Bw. Chen Zhihua, amesema Azimio la Ushirikiano Kati ya China na Afrika Katika Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi lililopitishwa kwenye Mkutano wa nane wa mawaziri wa Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC), limeanzisha uhusiano wa wenzi wa kimkakati wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kati ya  pande hizo mbili katika zama mpya, ambapo China na Afrika zitaimarisha ushirikiano wa kujenga uwezo katika suala hilo.

Akihutubia kongamano maalumu kuhusu kazi zijazo kufuatia mkutano huo lililofanyika hivi karibuni mjini Beijing, Bw. Chen Zhihua amesema katika muda mrefu uliopita, China na Afrika zimeshirikiana mara nyingi kwenye kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kuhifadhi mazingira. China imesaidia kuzijengea nchi za Afrika uwezo wa kukabiliana na changamoto hiyo kupitia njia mbalimbali zikiwemo kutoa teknolojia za saitelaiti, kuzisaidia kujenga vituo vya kuzalisha umeme kwa nishati ya jua, na kujenga kwa ushirikiano maeneo ya kielelezo ya utoaji mdogo wa kaboni. China pia imejitahidi kutoa msaada kwenye kutoa mafunzo kwa raslimali watu katika nyanja hiyo, na mpaka sasa imezisaidia nchi zaidi ya 30 za Afrika kutoa mafunzo hayo. Bw. Chen amesema, wakati wa kutoa mafunzo hayo, China kamwe haijichukulii kama mwalimu, bali inapenda kubadilishana na nchi za Afrika uzoefu, ujuzi na busara zake za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Bw. Chen ameeleza kuwa, kwa mujibu wa azimio hilo, China na Afrika zitapanua zaidi ushirikiano halisi kwenye nyanja hiyo, hasa katika sekta za nishati safi, matumizi ya teknolojia ya anga na anga za juu, kilimo, misitu, bahari, ujenzi wa miundombinu yenye utoaji mdogo wa kaboni, utabiri na utoaji tahadhari wa hali ya hewa, usimamizi wa mazingira, upunguzaji wa madhara ya maafa na uwezo wa kuhimili mabadiliko ya tabianchi, ili kukabiliana na changamoto hiyo kwa pamoja.

Bw. Chen Zhihua amesema, Wizara ya Ikolojia na Mazingira ya China itaharakisha utekelezaji wa miradi iliyosainiwa ya ushirikiano wa Kusini-Kusini na kati ya pande tatu wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, na kupanua zaidi uwekezaji kwenye miradi yenye utoaji mdogo wa kaboni katika sekta za nishati endelevu kama vile umeme wa nishati ya jua na upepo, teknolojia ya kupunguza matumizi ya nishati na teknolojia za hali ya juu. Mbali na hayo, China haitajenga miradi mipya ya kuzalisha umeme kwa makaa ya mawe nje ya nchi, ili kuzisaidia nchi za Afrika kurekebisha muundo wa nishati na kuboresha muundo wa viwanda.