Imani kubwa ya Wachina kwa serikali yao imethibitisha nini?
2022-01-27 13:58:07| CRI

Imani kubwa ya Wachina kwa serikali yao imethibitisha nini?_fororder_dcc451da81cb39dbaf3c18c77f10c12daa1830b6

Shirika kubwa zaidi la mahusiano ya umma duniani la Edelman, hivi karibuni limetoa ripoti ya mwaka 2022 ya “Edelman Trust Barometer”, ikionesha kuwa imani ya Wachina kwa serikali yao imefikia 91%, na kushika nafasi ya kwanza duniani.

Katika miaka ya karibuni, nchi za Magharibi zimekuwa zikiipaka matope serikali ya China, na kusema inapuuza haki za wananchi wake, lakini kwa nini Wachina wanazidi kuiamini serikali yao kuliko watu wa nchi za Magharibi, chanzo chake ni nini, na inathibitisha nini?

Mwaka 2017 na 2018, serikali ya China ilishika nafasi ya kwanza katika orodha ya “Edelman Trust Barometer” kuhusu imani ya watu kwa serikali yao. Mwaka huu, kwa mara nyingine tena, serikali ya China imeshika nafasi ya kwanza kwa alama ya asilimia 91, ambalo ni ongezeo la asilimia 9 kuliko mwaka uliopita, na ni kiwango cha juu zaidi katika mwongo mmoja. Kinyume kabisa na China, asilimia 39 tu ya Wamarekani ndio wana imani kwa serikali, pengo kati ya nchi hiyo na China limekuwa kubwa zaidi tangu kuanzishwa kwa ripoti hiyo ya Edelman.

Matokeo haya yanaweza kuwa jambo ambalo wanasiasa wa baadhi ya nchi za Magharibi haswa Marekani hawataki kuyaona, kwani mara kwa mara wanachochea mvutano katika uhusiano kati ya serikali ya China na wananchi wake, na hata wanatarajia “mapinduzi ya rangi” kutokea nchini China. Ripoti hiyo ya Edelman imewashangaza, kwa nini Wachina wana imani kubwa namna hii kwa serikali yao, na hii inamaanisha nini?

Imani kubwa ya Wachina kwa serikali yao inatokana na utekelezaji wa pande zote wa wazo la kiutawala la serikali inayoongozwa na Chama cha Kikomunisti cha China, ambalo linazingatia zaidi wananchi, ambapo inaonyesha kuwa, serikali ya China ni serikali halisi inayosimamia kikamilifu maslahi ya watu. Rais Xi Jinping wa China amesisitiza mara kwa mara kwamba, “matumaini ya watu ya kupata maisha bora ndio lengo letu.” Serikali ya China inazingatia maslahi ya watu, inazingatia uboreshaji na ustawi wa maisha ya watu, na wakati wote imejitolea kuhakikisha usalama na utulivu wa maisha ya watu. Tangu kutokea kwa janga la COVID-19, tofauti na baadhi ya nchi za Magharibi ambazo zimetumia janga hilo kama nyenzo ya kisiasa ya kushambulia wapinzani wao na kupata kura, zikipuuza maisha ya watu, serikali ya China imeweka umuhimu zaidi kwa usalama wa maisha ya watu, na kuchukua hatua madhubuti za kuzuia na kudhibiti janga hilo. Kutokana na hatua mwafaka za serikali, utaratibu wa kawaida wa maisha na kazi nchini China ulirejeshwa haraka, na kuongeza imani ya wananchi katika kushinda janga hilo.

Imani kubwa ya Wachina pia inatokana na juhudi kubwa za serikali za kustawisha tena taifa, ambapo inaonesha kuwa serikali ya China ni serikali inayoweza kuwaongoza watu wake kutimiza ndoto zao za maendeleo. Katika zaidi ya miaka mia moja iliyopita, kila Mchina ana ndoto ya kustawisha tena China. Historia na hali halisi vimewaambia Wachina kwamba ndoto hii inaweza kutimizwa tu chini ya uongozi wa serikali chini ya Chama cha Kikomunisti cha China. Katika miaka miwili iliyopita tangu kutokea kwa janga la COVID-19, uchumi wa nchi mbalimbali duniani umeathiriwa sana. Hata hivyo, China bado imepata mafanikio makubwa. Mwaka 2020, China ilikuwa nchi pekee ya uchumi mkubwa duniani ambayo ilitimiza ukuaji wa uchumi. Katika mwaka huo huo, China ilitangaza kuwa imeondokana na umaskini uliokithiri, na kutimiza lengo la kujenga jamii yenye maisha bora kwa pande zote, ambalo ni lengo lake la kwanza la miaka 100. Mwaka 2021, uchumi wa China ulikua kwa asilimia 8.1, ambacho ni kiwango cha juu zaidi katika mwongo uliopita, na pato la taifa kwa mtu lilifikia dola 12,500 za Marekani, ambayo ni karibu sana na kigezo cha dola 12,695 ili kuwa nchi yenye pato la juu kilichowekwa na Umoja wa Mataifa.

Serikali ya China inawaongoza wananchi wake kupiga hatua kubwa kuelekea lengo lake la pili la miaka 100, ambalo ni kujenga nchi ya kisasa ya kisoshalisti yenye ustawi, demokrasia na ustaarabu mkubwa.