Mkutano wa Viongozi wa Jumuiya ya Madola wapangwa kufanyika Juni nchini Rwanda
2022-02-01 16:32:10| cri

Sekretarieti ya Jumuiya ya Madola imetoa taarifa ikisema, Mkutano wa Wakuu wa Serikali za Jumuiya ya Madola (CHOGM) unaofanyika kila baada ya miaka miwili, ambao ulipangwa kufanyika Juni 2020 lakini uliahirishwa mara mbili kutokana na athari za COVID-19, sasa umepangwa kufanyika Juni 20 mjini Kigali nchini Rwanda.

Rais wa Rwanda Paul Kagame na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola Patricia Scotland, wametangaza wiki ya Juni 20 kama tarehe mpya iliyokubaliwa na nchi wanachama wa CHOGM. Kwenye taarifa yake rais Kagame amesema mkutano huo utakuwa muhimu katika kukabiliana na changamoto zinazotokana na janga la COVID-19 na kujenga uvumbuzi wa kiteknolojia na fursa za kiuchumi ili kutatua masuala mengine muhimu yanayowakabili wananchi.

Kwa upande wake Scotland amesema huu utakuwa mkutano wa kwanza kufanyika Afrika katika zaidi ya muongo mmoja na kuwa anafurahi kwamba familia ya wanajumuiya ya madola hatimaye itakutana tena miaka minne baada ya ule uliofanyika mjini London nchini Uingereza.