Iran yasubiri majibu kutoka Marekani kuhusu mazungumzo ya suala la nyuklia la Iran
2022-02-01 16:34:03| CRI

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Iran Saeed Khatibzadeh jana alisema, Iran imewasilisha pendekezo la maadishi kwenye mazungumzo ya pande husika za JCPOA, na inasubiri Marekani kutoa uamuzi wa kisiasa kuhusu masuala husika.

Khatibzadeh amesema mazungumzo kuhusu suala la nyuklia la Iran yanayofanyika mjini Vienna yamepata maendeleo, lakini hayajaafikiana kuhusu kuondoa vikwazo dhidi ya Iran, kwani inahitaji nchi za magharibi zinazoshiriki kwenye mazungumzo hayo kutoa uamuzi.

Amependekeza Marekani kuzingatia kujibu matakwa halali ya Iran, na kutotoa matakwa yanayokiuka makubaliano ya JCPOA.

Ameongeza kuwa, kama pande nyingine zinaweza kujibu matakwa ya Iran baada ya kurejeshwa kwa mazungumzo, huenda watafikia makubaliano ya kutegemeka na ya muda mrefu, na haihitaji kuweka muda wa mwisho wa mazungumzo.