Dunia yajumuika na China katika michezo ya Olimpiki ya majira ya baridi
2022-02-04 17:25:17| CRI

Dunia yajumuika na China katika michezo ya Olimpiki ya majira ya baridi_fororder_图像_2022-02-18_100612

Hatimaye mwaka mpya wa jadi wa China ambao ni mwaka wa chuimilia umefika! Mwaka huu umeanza kwa kishindo, matumaini na macho ya dunia yakielekezwa China. Kwa mara nyingine tena Beijing ni mwenyeji wa wageni kutoka pembe zote za dunia wanaojumuika kwa ajili ya olimpiki ya majira ya baridi maudhui yake yakiwa ni Pamoja kwa Mustakabali wa kesho.

Kwa miaka mitatu sasa, ulimwengu na walimwengu wametenganishwa kutokana na janga la Covid19. Robo tatu ya shughuli za kitaifa na kimataifa zilikwama katika kipindi hiki kila nchi ikijitahidi kupambana na kuenea kwa virusi vya corona. Mashindano ya Olimpiki ya majira ya baridi ya mwaka huu yanalenga kuleta mwamko mpya duniani kote. Washiriki, wafuatiliaji na watazamaji kote ulimwenguni wanajumuika tena, kufurahia na kutabasamu pamoja kwa ajili ya siku za usoni.

Wakati wa kukagua uwanja wa michezo hiyo jijini Beijing, rais Xi Jinping alisema 'Tunajiamini kuwa tatandaa mashindano ya kipekee ya Olimpiki yatakayoifurahisha dunia." Ulimwengu tayari unasubiri kuona haya.

Wakenya wamekuwa wakifuatilia maandalizi ya mashindano hayo na hivi sasa wako tayari kushabikia nchi na wachezaji wa nchi tofauti watakaoshiriki. Patrick Owuor mkufunzi wa michezo ya sarakasi jijini Nairobi ni moja wa wafuatiliaji wakubwa wa michezo duniani. Patrick pia aliishi China kuanzia mwaka wa 1985 akiwa na umri wa miaka kumi na mitano na kushiriki kwenye mashindano kadhaa. Anasema China inafahamika kwa ustadi wa hali ya juu kuandaa mashindano, na mashindano ya mwaka huu yatakuwa ya kipekee.

'Ulimwengu utarajie makubwa katika ulingo wa Michezo. Wachina huchukua muda kuandaa mambo yao kwa makini. Nina uhakika kuwa mashindano haya yatakuwa na mvuto wa kipekee kwa washiriki na sisi watazamaji, pia natazamia China kuzoa medali nyingi."

Daktari Luke Teroitich Ritok kutoka chuo cha Egerton kwenye kaunti ya Nakuru anasema licha ya janga la Corona kuitikisa dunia, michezo ya olimpiki ya majira ya baridi itaileta dunia pamoja na kuondoa hofu ya nchi kutenganishwa na hofu ya kusambaa kwa virusi vya Corona. "China ni nchi yenye teknolojia ya hali ya juu kuanzia kwa kupima hadi kutibu, walishinda virusi vya corona mapema sana. Mimi kama mpenzi wa michezo naamini kuwa hili janga haliwezi zuia dunia kutangamana, kwanza macho yote ya dunia yatakuwa Beijing" alisema bwana Teroitich.

Rais Xi alisema mashindano ya mwaka huu kando na kuleta Wachina na ulimwengu pamoja, yatatoa motisha kwa zaidi ya wachina milioni 300 kushiriki katika mashindano hayo kwa njia tofauti jambo analokubaliana nalo Hilda Juma mwanafunzi katika chuo Kikuu cha Nairobi.

"Mashindano ya kimataifa huwavutia watu wengi. Wale wanaoshiriki moja kwa moja bila kusahau wale wanaoshabikia pande tofauti. Sisi hapa Kenya na Afrika kwa jumla tutapata motisha wa kuimarisha viwango vyetu vya michezo tukitazama kile kinachoendelea China. Licha ya kuwa serikali ya China inalenga kudhibiti idadi ya watu watakaohudhuria, ukweli ni kwamba wale watakaokuwa wakitazama kwenye rungina, kufuatilia kwenye radio au kusoma habari za mashindano hayo watapata mshawasha wa kuendelea kushabikia michezo na hata kufanya mazoezi kwa manufaa ya afya yao." alisema Bi. Hilda.

Licha ya Afrika kutokuwa na majira ya baridi kali na theluji kama ilivyo kwenye nchi za Asia, Ulaya na Marekani na sehemu nyingine za dunia, jumla ya wanariadha sita kutoka nchi tano za Afrika watashiriki kwenye michezo ya Olimpiki ya majira ya mwaka huu. Fatuma Abdalla Fakii kutoka Zanzibar anasema mashindano ya mwaka huu ni nafasi kwa ulimwengu kujifunza mengi kutoka kwa majirani "Afrika tuna mengi ya kujifunza kutoka kwa michezo ya mwaka huu. Kwa kutazama tu tutaelewa umuhimu wa kuboresha viwango vyetu vya michezo na namna ya kuiga mshikamano wa nchi kama China"

Beijing umekuwa mji wa kwanza duniani kuandaa mashindano ya Olimpiki ya majira ya baridi na joto. Mashindano ya olimpiki ya majira ya joto yaliandaliwa mwaka wa 2008 na kuibuka mshindi kwa kupata medali 100, 51 zikiwa za dhahabu na wanatarajia kuvunja rekodi hiyo kwenye mashindano ya olimpiki ya majira ya baridi ya mwaka huu.