Mjumbe wa China alitaka Baraza la Usalama kutumia njia za busara na uwajibikaji zinapotoa vikwazo
2022-02-08 09:43:45| CRI

Mwakilishi wa kudumu wa China kwenye Umoja wa Mataifa Zhang Jun, jana Jumatatu alilitaka Baraza la Usalama kutumia njia za busara na uwajibikaji linapotoa vikwazo, wakati akizungumzia suala la vikwazo ilivyowekewa Korea Kaskazini na vikwazo vya upande mmoja.

Balozi Zhang amesema, huo ni msimamo wa kudumu wa China kwamba nchi zote wanachama wa Umoja wa Mataifa zinapaswa kubeba wajibu na kutekeleza kwa nia njema vikwazo vinavyoidhinishwa na Baraza la Usalama. Amesema kwa miaka 20 iliyopita kumekuwa na mwenendo wa kupanua mamlaka ya baraza katika kutoa vikwazo, ambapo athari zake mbaya za kibinadamu na za maisha ya watu haziwezi kufumbiwa macho, kwani pia vimeongeza uharibifu wa uchumi na shughuli za kijamii.

Aidha balozi Zhang amelisisitiza baraza hilo kwamba wanahitaji kuzingatia kwa makini namna wanavyochukua hatua ili kuboresha utekelezaji wa vikwazo wa Baraza la Usalama na kupunguza athari mbaya kwa nchi zinazowekewa vikwazo.