Tanzania yasaini mkataba na kampuni ya Kimataifa ya China CRRC ili kununua mabehewa 1,430 ya reli ya SGR
2022-02-10 09:32:37| CRI

Shirika la Reli Tanzania (TRC) limesaini mkataba na kampuni ya Kimataifa ya China CRRC ambayo inaendeshwa na serikali, ili kununua mabehewa 1,430 ambayo yatapelekwa kwenye reli ya kisasa ya SGR.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na TRC, mkataba huo, wenye thamani ya dola milioni 127.26 za Marekani, ulisainiwa Jumanne na Mkurugenzi Mkuu wa TRC Masanja Kadogosa na Meneja Mkuu msaidizi wa kampuni ya Kimataifa ya CRRC Tang Yunpeng huko jijini Dar es Salaam Tanzania. Kwenye taarifa hiyo Kadogosa amesema mkataba huo wa miezi 12 utajumuisha muundo, uzalishaji na upelekaji wa mabehewa 1,430 ya kusafirishia aina mbalimbali za mizigo.

Mabehewa hayo yatapelekwa Dar es Salaam mapema Februari mwaka 2023 baada ya kukamilika kwa ujenzi wa pili wa reli yenye urefu wa kilomita 422 kutoka Morogoro hadi Makutopora ambayo itaungana na sehemu ya reli inayotoka Dar es Salaam hadi Morogoro yenye kilomita 341, ambayo ujenzi wake umefikia asilimia 95.

Naye Tang amesema kampuni ya Kimataifa ya CRRC itahakikisha inapeleka mabehewa bora ya mradi wa SGR ndani ya kipindi cha makubaliano.