Kimbunga cha Batsirai chasababisha vifo vya watu 92 Madagascar
2022-02-10 09:26:47| CRI

Ripoti iliyotolewa jana usiku na Ofisi ya Usimamizi wa Hatari na Maafa (BNGRC) imesema kimbunga kikali cha tropiki kiitwacho Batsirai kilipita Madagascar tarehe 5 na 6 mwezi huu, na kusababisha vifo vya watu wasiopungua 92.

Ripoti hiyo imesema kati ya watu 92 waliokufa, 71 walitoka wilayani Ikongo jimboni Fitovinany, kusini mashariki mwa nchi hiyo. Ofisa wa BNGRC Bibi Carole Ray amesema vifo vya watu wa Ikongo vingi vimesababishwa na kuporomoka kwa nyumba na ongezeko la maji. Ingawa tahadhari ya usalama inatolewa kila siku, na hatua ya kuwaondoa watu kwa dharura imechukuliwa, lakini baadhi ya wakazi walikataa kuondoka kwenye makazi yao. Idadi ya vifo itaendelea kuongezeka baada ya taarifa nyingi kukusanywa.

Takwimu zimeonyesha kuwa watu zaidi ya laki 1.1 wameathiriwa na kimbunga nchini humo, na wengine 61,489 wamepoteza makazi yao.