Mawaziri wa biashara wa Umoja wa Ulaya wajadili ushirikiano wa kibiashara na AU, Marekani
2022-02-15 08:45:00| CRI

Mawaziri wa biashara kutoka Baraza la Mambo ya Nje la Umoja wa Ulaya wamejadili vipaumbele vya sera ya biashara ya umoja huo na ushirikiano kati yake na Umoja wa Afrika na Marekani.

Akiongea kwenye mkutano uliofanyika kuanzia Jumapili hadi Jumatatu huko Marseille nchini Ufaransa, mjumbe wa waziri wa biashara ya nje wa Ufaransa Bw. Franck Riester amesema nchi za Umoja wa Ulaya zinapaswa kuwa na uhuru wa kimkakati wa kuitikia matishio na changamoto za kiuchumi duniani, huku zikiheshimu malengo ya kulinda mazingira endelevu ya umoja huo.

Kamishna wa biashara wa Ulaya Valdis Dombrovskis amesema mkutano wa kilele kati ya Umoja wa Ulaya na Umoja wa Afrika unatakiwa kuleta makubaliano mapya kwa ajili ya mageuzi ya kidijitali kwenye uchumi wa Afrika na maeneo ya biashara huria, akisisitiza kuwa nchi za Afrika ni washirika wakuu kwa Umoja wa Ulaya.

Mawaziri hao pia walijadili ushirikiano kati ya Umoja wa Ulaya na Marekani, na jinsi pande hizo mbili zitakavyokabiliana na “hatari za pamoja”, na kutatua masuala yaliyopo kwenye biashara kati yao.