Umoja wa Mataifa na wadau wazindua mpango wa kibinadamu wa mwaka 2022 kwa Mali
2022-02-15 09:22:36| CRI

Ofisi ya Uratibu wa Mambo ya Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa OCHA, Umoja wa Mataifa na wadau wake wa kibinadamu wamezindua mpango wa mwitikio wa kibinadamu wa mwaka 2022 kwa Mali wenye thamani ya dola milioni 686 za kimarekani.

Ofisi hiyo imesema mpango huo unalenga kuwasaidia watu zaidi ya milioni 5.3 wenye hali duni zaidi kati ya watu milioni 7.5 wanaohitaji msaada wa kibinadamu, na kiwango cha mahitaji ni cha juu zaidi kuliko wakati wowote tangu mwaka 2012.

Kutokana na kuongezeka kwa machafuko katika sehemu ya kati ya nchi hiyo, hali ya kibinadamu ilizorota mwaka jana. Msukosuko wa usalama sasa umeenea hadi sehemu ya kusini. Vurugu na athari za mabadiliko ya tabianchi vimeongeza idadi ya watu wenye hatari ya kukosa chakula. Watu wapatao milioni 1.8 watahitaji msaada wa chakula kwa mwaka huu, ikiongezeka kwa asilimia 51 kuliko mwaka 2021.