Wang Yi: Pande zote zinatakiwa kujitahidi kufikisha amani badala ya kutoa tisha ya vita
2022-02-19 23:36:14| cri
Waziri wa mambo ya nje wa China Bw. Wang Yi alihudhuria mkutano wa 58 wa usalama wa Munich kwa njia ya video Februari 19 na kutoa hotuba, pia alieleza msimamo wa China kuhusu upanuzi wa Jumuiya ya NATO, usalama wa Ulaya na hali ya Ukraine.

Wang Yi alisema, vita vya baridi tayari vimemalizika, Jumuiya ya NATO ikiwa ni tunda la vita vya baridi, inatakiwa kufanyiwa mabadiliko kwa kufuatia hali ilivyo sasa. Kama NATO ikishikilia kupanua wigo wake kwa kuelekea Mashariki, je hatua hiyo ama kweli inasaidia amani na utulivu barani Ulaya katika muda mrefu? Hilo ni swali linastahili watu wa Ulaya wafikirie kwa makini. Wang Yi alisisitiza kuwa, mamlaka ya nchi, uhuru wake na ukamilifu wa ardhi yake vyote vinapaswa kuheshimiwa na kulindwa, hii ni kanuni ya kimsingi katika uhusiano wa kimataifa inayokubaliwa na Umoja wa Mataifa, pia ni msimamo wa kikanuni unaofuatwa na China katika kushughulikia masuala ya kimataifa, likiwemo suala la Ukraine. Wale wanaoikosoa China katika suala hilo wanafanya makusudi kupotosha msimamo wa China. Waziri huyo akifafanua msimamo wa China katika suala la Ukraine alisema, pande zote zinapaswa kurudi katika Makubaliano ya Minsk, kwani yalifikishwa na pande husika kwa njia ya mazungumzo, na pia yalikubaliwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Makubaliano hayo ni njia pekee ya kutatua suala la Ukraine. Wang Yi alisema, imefahamika kuwa, Russia na Umoja wa Ulaya zote zinaunga mkono makubaliano hayo. Na waziri wa mambo ya nje wa Marekani Bw Antony Blinken alipoongea na Wang Yi hivi karibuni kwa simu, alieleza uungaji mkono wa Marekani kwa makubaliano hayo. Kwa hivyo, Bw Wang aliuliza, mbona pande zote haziwezi kukaa pamoja na kujadiliana ipasavyo, ili kutunga ratiba na hatua halisi za kutekeleza makubaliano hayo? Wang Yi alisisitiza kuwa, hivi sasa cha muhimu zaidi ni kwamba, pande zote zinabeba wajibu wa kujitahidi kufikisha amani, badala ya kuongeza hali ya wasiwasi na kutoa tisha la vita.