Putin aidhinisha "operesheni maalum ya kijeshi" katika eneo la Donbass
2022-02-24 16:08:56| Cri

Rais wa Russia Vladimir Putin leo Alhamisi ameidhinisha "operesheni maalum ya kijeshi" katika eneo la Donbass, na Ukraine imethibitisha kuwa maeneo yote ya kijeshi yaliyolengwa kote nchini yanashambuliwa.

Akilihutubia taifa kwa njia ya televisheni Putin amesema mipango yao haijumuishi uvamizi wa maeneo ya Ukraine, na kwamba hawatalazimisha kwa nguvu chochote kile au kwa mtu yeyote yule na kubainisha kuwa hatua ya Russia ni kujibu "vitisho vya kimsingi" vya Jumuiya ya Kujihami ya Nchi za Magharibi (NATO) ambavyo vimepanuka hadi Ulaya Mashariki na kuleta miundombinu yake ya kijeshi karibu na mipaka ya Russia.

Putin alitoa wito kwa watu wote wanaoishi katika eneo la Ukraine "kuamua kwa hiari mustakabali wao na wa watoto wao.”

Putin Jumatatu alitia saini amri mbili zinazoitambua "Jamhuri ya Watu wa Lugansk" na "Jamhuri ya Watu wa Donetsk" kama nchi huru na zinazojitawala na kupeleka vikosi vya "kulinda amani" katika sehemu hizo mbili.