Siku ya kimataifa ya wanawake na wasichana katika Sayansi na Maisha ya wanawake yabadilishwa kutokana na teknolojia
2022-02-25 08:20:10| Cri

Februari 11 kila mwaka ni siku ya kimataifa ya wanawake na wasichana katika Sayansi. Lengo likiwa ni fursa kwa wote kuchukua msimamo kwa ajili ya wasichana na wanawake katika sekta hii muhimu.

Katika kuadhimisha siku hii iliyopitishwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwaka 2015, Shirika la Umoja wa Mataifa la elimu sayansi na utamaduni, UNESCO limesema wasichana wanaendelea kukumbwa na ubaguzi, vikwazo vya kijamii na kitamaduni ambavyo vinawazuia kupata elimu na fedha za kufanya utafiti na kuwazuia kuingia katika kazi zitokanazo na masomo ya sayansi na hivyo kuwakwamisha kufikia uwezo wao kikamilifu.

UNESCO inasema idadi ya wanawake katika utafiti wa sayansi na uamuzi bado ni ndogo. Hii inaleta kikwazo kikubwa katika juhudi za kufikia malengo ya maendeleo endelevu, SDGs. Lakini taswira inapaswa kubadilika na hii itawezekana iwapo wasichana na wanawake watapata fursa, aidha kundi hili lipewe motisha ili kuhakikisha kwamba sekta ya sayansi inawakilishwa na wanawake vilivyo. Hivyo basi leo hii katika ukumbi wa wanawake tutaangalia maisha ya wanawake yalivyobadilika kutokana na sayansi na teknolojia.