Rais wa Marekani atangaza vikwazo zaidi dhidi ya Russia
2022-02-25 08:44:34| CRI

Rais wa Marekani Joe Biden ametangaza vikwazo zaidi dhidi ya Russia na kusema atapeleka askari zaidi barani Ulaya, wakati mgogoro nchini Ukraine ukibadilika.

Akizungumza katika Ikulu ya nchi hiyo jana, rais Biden amesema hatua hizo mpya zitalenga benki muhimu za Russia, kuweka kikomo kwa uwezo wa nchi hiyo kufanya biashara kwa kutumia dola ya Marekani, Euro, Pauni na sarafu ya Japan Yen, na pia kuzuia nchi hiyo kuagiza teknolojia ya juu na uwezo wa kuongeza nguvu ya jeshi lake.

Pia rais Biden amesema ameidhinisha kupelekwa kwa vikosi vya jeshi la anga na la nchi kavu katika eneo la mashariki mwa Ulaya, na kuongeza uwezo wa jeshi la Marekani kupelekwa Ujerumani, ikiwa ni sehemu ya majibu ya Jumuiya ya Kujihami ya Nchi za Magharibi (NATO).

Wakati huohuo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia Sergei Lavrov amesema, Marekani na NATO wamevunja ahadi yao, wamekataa kutekeleza Makubaliano ya Minsk, na kukiuka Azimio namba 2202 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Naye rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine ametangaza jana kwamba, nchi hiyo imeamua kuvunja uhusiano wa kidiplomasia na Russia.