Rais Xi Jinping wa China afanya mazungumzo na mwenzake wa Russia
2022-02-25 20:29:21| cri

Rais Xi Jinping wa China leo ijumaa amefanya mazungumzo kwa njia ya simu na Rais Vladimir Putin wa Russia, na kubadilishana naye maoni kuhusu hali ya sasa ya Ukraine.

Rais Xi amesisitiza kuwa China inaunga mkono Russia na Ukraine kutatua suala hilo kwa njia ya mazungumzo, akibainisha kuwa hali ya hivi karibuni mashariki mwa Ukraine imebadilika sana, na kuleta wasiwasi mkubwa katika jumuiya ya kimataifam, na kuwa msimamo wa China kuhusu suala hilo unaendana na hali halisi.

Rais Xi amezitaka pande zote kuachana na mawazo ya vita baridi, kuheshimu na kuzingatia umuhimu wa masuala halali ya wasiwasi wa usalama wa kila upande, na kujitahidi kwa utaratibu kuzingatia usalama wa Ulaya kwa njia yenye uwiano, ufanisi na endelevu kwa njia ya mazungumzo.

Rais Xi amesema China iko tayari kufanya kazi na pande zote katika jumuiya ya kimataifa ili kuhimiza usalama wa pamoja, wa kina, na endelevu ili kuimarisha mfumo wa kimataifa unaozingatia Umoja wa Mataifa na utaratibu wa kimataifa unaosimamiwa na sheria za kimataifa.

Rais Putin amesisitiza kuwa Marekani na NATO kwa muda mrefu zimekuwa zikipuuza masuala halali ya usalama ya Russia, mara kwa mara wakirudia ahadi zao na kuendelea kuhimza majeshi yao kusonga mbele kuelekea mashariki, jambo ambalo ni changamoto kwa usalama wa Russia. Rais Putin amemwambia Rais Xi kuwa Russia iko tayari kufanya mazungumzo ya ngazi ya juu na Ukraine.

Rais Xi kwa mara nyingine tena ametoa shukrani zake kwa Rais Putin kwa kuhudhuria sherehe za ufunguzi wa michezo ya Olimpiki ya majira ya baridi ya Beijing 2022 na kuwapongeza wanariadha wa Russia kwa kuchukua nafasi a pili katika jedwali la medali.

Rais Putin amewapongeza watu wote wa China kwa kuandaa kwa mafanikio michezo ya Olimpiki ya majira ya baridi ya Beijing, na wanamichezo wa China kufanya vizuri.