Ukraine kutuma ujumbe kwa ajili ya kufanya mazungumzo na Russia kwenye mpaka wa Belarus
2022-02-28 14:05:11| CRI

Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine jana alitumia mitandao ya kijamii akisema Ukraine inakubali kufanya mazungumzo na Russia kwenye mpaka kati ya Belarus na Ukraine ulioko karibu na Mto Pripyat.

Makubaliano hayo ya kufanya mazungumzo yalifikiwa wakati wa mazungumzo ya simu kati ya rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine na mwenzake wa Belarus Alexander Lukashenko. Ofisi ya rais ya Ukraine inasema Lukashenko amebeba jukumu la kuhakikisha kuwa ndege, helikopta na makombora yote yaliyoko kwenye ardhi ya Belarus yatakuwa ardhini wakati wa ziara, mazungumzo na kurudi kwa ujumbe wa Ukraine.

Hata hivyo, Shirika la habari la Russia limemnukuu mwanahabari wa Shirika la habari la Sputnik akisema kuwa hadi sasa mazungumzo kati ya Russia na Ukraine bado hayajafanyika, lakini yatafanyika haraka. Ujumbe wa Ukraine bado haujafika mahali pa mazungumzo, ambapo sehemu ya awali ya mazungumzo imebadilishwa kutokana na madai ya Ukraine.