Kenya kuvutia nchi za Afrika Mashariki kutumia bandari ya Lamu iliyojengwa na China ili kuendeleza biashara ya kimataifa
2022-03-02 09:46:04| CRI

Kenya imesema itavutia mataifa ya Afrika Mashariki yasiyo na bahari kutumia bandari yake ya Lamu iliyojengwa na China ili kuyawezesha kuendeleza biashara yao ya kimataifa.

Mkurugenzi mkuu na Afisa Mtendaji Mkuu wa mradi wa kuimarisha uchukuzi na miundombinu wa LAPSSET, Stephen Ikua ameliambia kongamano la Afrika lililofanyika Nairobi, Kenya kwamba bandari ya pili ya kibiashara nchini Kenya ina uwezo wa kushughulikia meli kubwa ikilinganishwa na bandari ya Mombasa, kutokana na kina chake kikubwa cha maji.

Amebainisha kuwa rasilimali nyingi za madini na kilimo za Sudan Kusini sasa zinaweza kusafirishwa kwa ufanisi kupitia bandari ya Lamu, na kuongeza mapato ya nchi ambayo inategemea zaidi uzalishaji wa mafuta ghafi.