Katibu mkuu wa NATO asisitiza jitihada za kidiplomasia katika kutatua mgogoro wa Ukraine
2022-03-02 09:42:43| CRI

Katibu mkuu wa Shirika la Kujihami la Mataifa ya Magharibi (NATO) Bw. Jens Stoltenberg jana alisisitiza kufanywa juhudi za kidiplomasia ili kutatua mgogoro unaoendelea wa Ukraine.

Stoltenberg alisema hayo kwenye mkutano na wanahabari uliowashirikisha waziri mkuu wa Estonia Bibi Kaja Kallas na waziri mkuu wa Uingereza Bw. Boris Johnson katika kituo cha kijeshi cha Tapa kilichoko kaskazini mwa Estonia.

Stoltenberg ametoa wito wa kusimamisha vita mara moja nchini Ukraine, kuondoa vikosi vya Russia na kufanya jitihada za kidiplomasia. Amesema katika wiki kadhaa zilizopita, wameongeza nguvu ya ulinzi angani, ardhini na baharini ili kukabiliana na mashambulizi ya Russia dhidi ya Ukraine. Ameongeza kuwa Uingereza, Marekani na nchi washirika wengine zinatuma maelfu ya askari katika sehemu ya mashariki ya shirika la NATO, ambalo ni shirika la ulinzi lisilotaka kupambana na Russia.