Mawaziri wa mambo ya nje wa China na Ukraine wazungumza kwa simu
2022-03-02 09:49:46| CRI

Mjumbe wa Baraza la Taifa la China na Waziri wa Mambo ya Nje Wang Yi amefanya mazungumzo kwa njia ya simu kufuatia ombi la Waziri wa Mambo ya Nje wa Ukraine Dmytro Kuleba.

Kwenye mazungumzo yao yaliyofanyika jana, Kuleba alimueleza Wang kuhusu duru ya kwanza ya mazungumzo kati ya Ukraine na Russia, akisema kuwa kumalizika kwa mapigano hayo ndio kipaumbele cha kwanza cha Ukraine. Alisema Ukraine inakubali utatuzi wa suala la sasa kwa njia ya mazungumzo na kuangalia mazungumzo yake na Russia kwa dhati, akiongeza kuwa licha ya matatizo ya sasa, upande wa Ukraine upo shwari na tayari kusukuma mbele mazungumzo hayo.

Kuleba alisema China imechukua nafasi ya kiujenzi katika suala la Ukraine, na kwamba Ukraine iko tayari kuimarisha mawasiliano na upande wa China na kutarajia upatanishi wa China katika kufikia usimamishaji mapigano.

Kwa upande wake, Wang alisema hali ya Ukraine imebadilika kwa kasi, na China inasikitika kuzuka kwa mgogoro kati ya Ukraine na Russia na inajali sana madhara kwa raia. Amesema msimamo wa msingi wa China kuhusu suala la Ukraine uko wazi na imara ya kwamba China daima inaheshimu uhuru na ukamilifu wa ardhi za nchi zote. Kuhusu mgogoro wa sasa, China inatoa wito kwa Ukraine na Russia kutafuta suluhu kupitia mazungumzo, na kuunga mkono juhudi zote za kiujenzi za kimataifa katika kutafuta suluhu ya kisiasa.