Wajumbe wa Russia wawasili kwa duru ya pili ya mazungumzo na Ukraine
2022-03-03 10:11:14| CRI

Ujumbe wa Russia umefika mahali ambapo duru ya pili ya mazungumzo kati ya Russia na Ukraine inatarajiwa kufanyika.

Shirika la habari la Russia RIA Novosti liliripoti likimnukuu msaidizi wa rais wa Russia Vladimir Medinsky, mkuu wa ujumbe wa Russia kwenye mazungumzo hayo, akisema upande wa Ukraine unatarajiwa kuwasili kesho asubuhi, na pande zote mbili zinatarajiwa kukutana huko Belovezhskaya Pushcha kwenye mpaka wa Belarus na Poland.

Medinsky alisema Russia na Ukraine zilikubaliana pamoja juu ya eneo la duru ya pili ya mazungumzo, akiongeza kuwa jeshi la Russia limeweka ukanda salama ili kuruhusu ujumbe wa Ukraine kupita katika ardhi ya Ukraine. Uwezekano wa kusitisha mapigano utajadiliwa wakati wa mazungumzo.

Wakati huohuo, Wizara ya Mambo ya Nje ya Ukraine Jumatano ilitoa taarifa kwenye Facebook ikisema, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ukraine Dmytro Kuleba na mwenzake wa Marekani Antony Blinken walijadili vikwazo vipya dhidi ya Russia katika mazungumzo yao ya simu.

Kuleba na Blinken pia walizungumza juu ya usambazaji mpya wa silaha za kujilinda kwa Ukraine. Kuleba alisisitiza kuwa Ukraine imejitolea kutafuta njia za kidiplomasia za kusuluhisha mzozo na Russia, lakini washirika wa Ukraine lazima waonyeshe umoja katika kuongeza shinikizo kwa Russia "hadi Moscow itakapoonyesha utayari wake kwa mazungumzo ya kiujenzi."