Shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa (WFP) limeonya kuwa eneo la Pembe ya Afrika linakabiliwa na ukame mbaya zaidi tangu mwaka 1981, na takriban watu milioni 13 wanakumbwa na njaa.
Katika miaka ya hivi karibuni, China imetuma wataalamu wengi wa kilimo barani Afrika ili kulisaidia bara hilo kushughulikia usalama wa chakula. Hivi karibuni, WFP imezindua mpango wa kukabiliana na ukame katika Pembe ya Afrika, ili kutoa msaada wa chakula kwa watu wanaoathirika na ukama katika eneo hilo. Takwimu zilizotolewa na shirika hilo zinaonesha kuwa, upungufu wa mvua kwa majira matatu mfululizo umesababisha kukauka kwa mazao na vifo vya mifugo, na uhaba wa maji na malisho umewalazimisha watu wengi kukimbia makazi yao. Inakadiriwa kuwa takriban watu milioni 13 katika eneo hilo watakabiliwa na njaa kali katika robo ya kwanza ya mwaka huu.
Eritrea pia inakumbwa na ukame, na ili kuisaidia nchi hiyo kukabiliana na maafa hayo, China imetuma vikundi kadhaa vya wataalam wa kilimo nchini humo. Mkuu wa kikundi cha tatu cha wataalam wa kilimo kilichopelekwa na China nchini Eritrea Bw. Liu Yunmin, amesema nchi hiyo inaweza kujitosheleza chakula kwa karibu 65% tu, na nyingine zinategemea msaada wa kimataifa. Kulingana na uzoefu wake wa miaka mingi wa kufanya kazi barani Afrika, mbinu ya kimsingi anayopanga kuchukua ni kuhifadhi baadhi ya magugu ili kuzuia kupotea kwa udongo. Licha ya hayo, wakati wa majira ya mvua, atajaribu kuwahimiza wakulima kuchimba visima ili kuhifadhi maji kwa ajili ya majira yasiyo na mvua.
Kikundi cha tatu cha wataalam wa kilimo kutoka China kitafanya kazi nchini Eritrea kwa miaka miwili, ambapo wataalam hao watafanya majaribio ya kiteknolojia katika mazao ya kunde, matunda, mazao ya mafuta na mengineyo, na kutoa mafunzo kwa wakulima nchini humo.
Bw. Liu aliyewahi kufanya kazi katika nchi kadhaa barani Afrika, zikiwemo Nigeria, Ethiopia na sasa Eritrea, wakati janga la COVID-19 bado linakabili Pembe ya Afrika, ameamua kwenda Eritrea ili kuisaidia nchi hiyo kukabiliana na changamoto ya njaa.
Eritrea ilikuwa kituo cha kwanza cha ziara ya Waziri wa Mambo ya Nje wa China Wang Yi barani Afrika mwanzoni mwa mwaka huu. Kutuma wataalam wa kilimo barani Afrika ni moja ya mafanikio muhimu ya ziara hiyo, na pia ni utekelezaji wa makubaliano yaliyofikiwa katika mkutano wa nane wa mawaziri wa Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika uliofanyika mwishoni mwa Novemba mwaka jana. Mkutano huo ulipendekeza kuwa, China itashirikiana kwa karibu na nchi za Afrika ili kutekeleza kwa pamoja “Miradi Tisa”, ukiwemo mradi wa kilimo na kupunguza umaskini. Kufuatia mradi huo, China itatekeleza hatua 10 za kuhimiza ushirikiano katika masuala la kilimo na kupunguza umaskini, na itatuma wataalam 500 wa kilimo barani Afrika.
Kwenye semina ya utekelezaji wa makubaliano yaliyofikiwa katika Mkutano wa 8 wa Mawaziri wa FOCAC iliyofanyika hivi karibuni mjini Beijing, Mkuu wa Idara ya Mambo ya Afrika iliyo chini ya Wizara ya Mambo ya Nje ya China Bw. Wu Peng, alisema, China imejiandaa kubadilishana uzoefu na nchi za Afrika katika masuala ya kilimo, na pia iko tayari kutoa mafunzo kwa wataalam wa Afrika. Ameongeza kuwa China pia imefungua njia ya kijani kwa ajili ya mazao ya Afrika kuuzwa nchini China, ambayo itasaidia nchi za Afrika kupanua mauzo ya nje ya mazao ya kilimo, na kuendeleza kilimo.