Vikosi vya usalama vya Nigeria vyawaua zaidi ya watu 200 wenye silaha
2022-03-03 10:10:29| CRI

Zaidi ya watu 200 wenye silaha waliuawa wakati wa operesheni ya pamoja ya vikosi vya usalama vya Nigeria katika jimbo la Niger kaskazini ya kati mwa nchi hiyo kati ya Jumapili na Jumanne.

Akihutubia mkutano na wanahabari huko Minna, mji mkuu wa jimbo hilo, kamishna wa serikali ya jimbo Emmanuel Umar alisema maafisa wawili wa usalama walikufa katika operesheni huku wachache wakipata majeraha ya aina mbalimbali.

Alisema watu wenye silaha waliuawa katika maeneo ya Mariga, Wushishi, Mokwa na Lavun katika jimbo hilo, akibainisha kuwa zaidi ya pikipiki 100, ng'ombe kadhaa walioibiwa, na silaha na risasi zilipatikana kutoka kwa majambazi.

Umar aliwaambia waandishi wa habari kuwa baadhi ya watu waliokuwa wamejihami kwa bunduki walikimbia wakiwa na majeraha kadhaa na walikuwa wamejificha, huku akitoa wito kwa umma kuripoti mgeni yeyote katika jamii zao kwa vyombo vya usalama kwani vita hivyo si vya serikali pekee.