Michezo ya Olimpiki ya Majira ya Baridi ya Beijing yachangia juhudi za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi duniani
2022-03-03 14:28:25| cri

Michezo ya Olimpiki ya Majira ya Baridi ya Beijing yachangia juhudi za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi duniani_fororder_VCG111365855580

Michezo ya Olimpiki ya Majira ya Baridi ya Beijing imefungwa kwa mafanikio makubwa. Beijing ambao ni mji wa kwanza ulioandaa  Michezo yote ya Olimpiki ya Majira ya Joto na ya Baridi duniani, kwa mara nyingine tena iliishangaza dunia. Kauli mbiu ya michezo hii ni “Pamoja: Kwa Mustakabali wa Pamoja”.

Katika Michezo hii, kuanzia maandalizi ya awali ya kumbi hadi uendeshaji na usimamizi wa shughli za baadaye, China imezingatia dhana ya maendeleo endelevu ya kijani, na kuchangia juhudi za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi duniani.

Tangu mwanzo wa maandalizi ya Michezo hiyo, China ilipanga na kusimamia kwa kina ujenzi na ukarabati wa kumbi za michezo, kwa kutumia kikamilifu kumbi zilizopo tayari zilizotumika katika Michezo ya Olimpiki ya Majira ya Joto ya mwaka 2008, na kupunguza ujenzi wa kumbi mpya, ili kupunguza matumizi ya nishati na utoaji wa uchafu kwa mazingira. Uwanja wa Taifa wa Michezo ulitumika kufungua na kufunga Michezo ya Olimpiki ya mwaka 2008, na wakati huu tena, umetumiwa katika hafla hizo mbili. Jumba la Uogeleaji la “Water Cube” lilibadilishwa kuwa “Ice Cube”, na kutumika kama ukumbi wa mashindano ya mchezo wa Curling. Zaidi ya hayo, miundombinu mingi mjini Beijing iliyojengwa wakati wa Michezo ya Olimpiki ya Beijing ya mwaka 2008 pia umetumika, kama vile reli chini ya ardhi ya mstari wa 8 na 10, pamoja na vifaa vya usambazaji wa umeme na maji.

Mbali na kutumia vizuri miundombinu ya Michezo ya Olimpiki ya Majira ya Joto ya mwaka 2008, Michezo ya Olimpiki ya Majira ya Baridi ya Beijing pia ilizingatia sana kutumia majengo na vifaa vingine vilivyopo tayari, ili kupunguza uwekezaji katika ujenzi mpya. Jukwaa la Kuruka juu ya Theluji la Shougang ni moja ya kumbi zinazovutia zaidi katika Michezo hiyo. Zamani ilikuwa Kiwanda cha Chuma cha Beijing, na baadaye kilibadilishwa na kuwa bustani ya michezo, utamaduni, biashara na utalii.

China pia imetunga vigezo vya kutathmini majumba na viwanja vya kijani vya michezo, ambavyo ni vigezo vya kwanza vya aina hiyo duniani, na kutumia teknolojia mpya zaidi za kutengeneza barafu na theluji.

Kwa kufuata dhana ya Michezo ya Olimpiki ya kijani, China imetumia sana nishati ya upepo na jua, na kuandaa Michezo ya Olimpiki ya kwanza katika historia ambayo umeme uliotumiwa wote umezalishwa kwa nishati safi. Aidha, jumla ya magari 816 yanayotumia nishati ya hidrojeni yametumika katika Michezo ya Olimpiki ya Majira ya Baridi ya Beijing. Magari hayo yanaweza kupunguza utoaji wa hewa ya kaboni kwa takriban kilo 70 kwa kilomita 100.

Mabadiliko ya tabianchi duniani ni mojawapo ya changamoto kubwa zaidi zinazokabili binadamu. China kwa mara nyingine imedhihirisha dhamira na uwezo wake wa kukabiliana na changamoto hiyo. Licha ya kuandaa vizuri Michezo ya Olimpiki, China imezingatia sana dhana ya maendeleo endelevu ya kijani, na kuchangia urithi wa kipekee kwa maendeleo ya Michezo ya Olimpiki Duniani.