Putin asema operesheni ya Russia nchini Ukraine inakwenda kama ilivyopangwa
2022-03-04 10:37:25| CRI

Rais Vladimir Putin wa Russia amesema operesheni maalum ya kijeshi ya nchi hiyo nchini Ukraine inaendelea kulingana na ratiba na mpango.

Putin alisema katika mkutano na wajumbe wa kudumu wa Baraza la Usalama la Russia kuwa kazi zote zilizopangwa zinatimizwa kwa mafanikio. Aliwaambia maafisa wakuu wa nchi hiyo kuwa wanajeshi na maofisa wa Russia "wanapambana kwa ujasiri" na "wanapigana kwa uthabiti, wakiwa na ufahamu kamili wa haki ya kazi yao."

Alisema operesheni hiyo inalenga kuondoa vitisho vilivyosababishwa na nchi za Magharibi katika miaka ya hivi karibuni kwenye mipaka ya Russia, vikiwemo vitisho vya silaha za nyuklia.

Wizara ya Ulinzi ya Russia ilitangaza Jumatano kwamba wanajeshi 498 wa Russia wameuawa wakati wa operesheni maalum ya kijeshi nchini Ukraine iliyoanza Februari 24.