Rais Xi Jinping awataka maofisa vijana wawe na imani thabiti na kuchapa kazi
2022-03-05 16:47:37| cri

Rais Xi Jinping wa China amewataka maofisa vijana kuimarisha maadili na imani zao, kutekeleza kwa vitendo mtazamo sahihi kuhusu utendaji wao, na kufanya kazi kwa bidii kwa ajili ya mambo ya chama na umma.

Rais Xi ambaye pia katibu mkuu wa Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China (CPC) aliyasema hayo alipokuwa akihutubia sherehe za ufunguzi wa programu ya mafunzo kwa maofisa vijana na wenye umri wa kati katika chuo cha kamati kuu ya Chama.

Rais Xi amesisitiza umuhimu kwa maofisa vijana kuendeleza imani thabiti ya U-marx na kujitahidi kufikia maadili ya ukomunisti na ujamaa wenye umaalum wa China. Amesema hizo ni juhudi za maisha yote na sio za muda mfupi, katika kuimarisha maadili na imani. Amewataka kuzingatia kwa dhati nidhamu ya chama na sheria, na kulinda uadilifu wao dhidi ya rushwa katika kila kipengele cha maisha na kazi zao.

Rais Xi pia amewakumbusha maofisa hao kufanya kazi kwa ajili ya maendeleo ya umma na kwamba hayo ndio mafanikio yao makubwa ya kisiasa. Alisema, wakati wa kupanga na kutekeleza mipango, wanapaswa kuwa na dhamira ya dhati kwa malengo ya msingi ya Chama, ya kuwatumikia wananchi kwa moyo wote, na kwa kanuni kwamba maendeleo ni ya wananchi, yanawategemea wananchi, na matunda yake yanatakiwa kuwanufaisha wananchi.