Wang Yi asema China siku zote inasimama kwenye mwelekeo sahihi wa maendeleo ya kihistoria
2022-03-07 17:08:48| cri

Waziri wa Mambo ya Nje wa China Wang Yi leo amesema wakati dunia ikikabiliwa na misukosuko na mabadiliko, China daima imekuwa ikiwakilisha utulivu na nguvu chanya, na siku zote imekuwa ikisimama kwenye mwelekeo sahihi wa maendeleo ya kihistoria.

Amebainisha kuwa China itaendelea kutilia maanani dunia, kubeba wajibu wake, kunyanyua juu bango la amani, maendeleo, ushirikiano na kunufaishana, kuhimiza ujenzi wa uhusiano wa kimataifa wa aina mpya na kuhimiza ujenzi wa jumuiya ya binadamu yenye hatma ya pamoja.

Akijibu maswali kwenye mkutano na wanahabari wa Kikao cha Tano cha Bunge la 13 la Umma la China, Wang Yi amesema kwamba sasa dunia haina utulivu, na mabadiliko makubwa ambayo hayajawahi kushuhudiwa katika karne nzima yanatokea. Ameongeza kuwa ili kudumisha hali ya umwamba, baadhi ya nchi zenye nguvu kubwa zimeleta Mawazo ya Vita Baridi na kuunda kambi ya makabiliano, ambayo imeongeza zaidi machafuko na migawanyiko na kufanya dunia ambayo tayari ipo kwenye matatizo kuwa na matatizo zaidi.