Wang Yi: Ulaya yahimizwa kuwa na uelewa huru na usio na upendeleo kuhusu China
2022-03-07 17:35:24| cri

Waziri wa Mambo ya Nje Bw. Wang Yi amesema China daima imekuwa ikiutazama uhusiano kati ya China na Umoja wa Ulaya kwa mtazamo wa kimkakati na wa muda mrefu, na inatumai kuwa Ulaya itakuwa na uelewa huru na usio na upendeleo kuhusu China, kufuata sera chanya na ya kuangalia hali halisi kuhusu China, na kuungana na China kupinga mawazo ya kuleta "Vita Baridi Mpya" na kulinda na kutekeleza kivitendo sera ya pande nyingi.

Akijibu maswali kuhusu uhusiano kati ya China na Umoja wa Ulaya katika mkutano na waandishi wa habari kando ya Mkutano wa Tano wa Bunge la 13 la Umma la China, Wang Yi alisema kuwa China na Ulaya ni nguvu kuu mbili za kulinda amani ya dunia, ni masoko mawili makuu ya kukuza maendeleo ya pamoja, na pia ni nchi mbili zilizostaarabika zaidi zinazochochea maendeleo ya binadamu. Uhusiano wa China na Umoja wa Ulaya haulengi, hautegemei, wala kudhibitiwa na upande wa tatu. Pande mbili zinafanya mazungumzo na ushirikiano katika msingi wa kuheshimiana na kunufaishana, jambo ambalo litachangia nguvu tulivu kwa hali ya dunia yenye misukosuko mbalimbali.

Wang Yi amesisitiza kuwa sera ya China kuhusu Ulaya bado ni tulivu na thabiti, na haitabadilishwa kutokana na tukio moja moja. China itaendelea kuunga mkono Ulaya kuwa na uhuru na kujiamulia mambo, pamoja na mshikamano na ustawi wa Umoja wa Ulaya. Pande hizo mbili zinapaswa kusimamia vyema ajenda muhimu za kisiasa kama vile mkutano wa viongozi wa China na Umoja wa Ulaya, kuimarisha kuungana kimkakati, kupanua ushirikiano wa kivitendo, kuendeleza uratibu wa pande nyingi, kuimarisha mawasiliano ya watu na utamaduni, kudhibiti ipasavyo tofauti, na kushikana mikono kufanya mambo mazuri na yenye maana kwa dunia.