Russia na Ukraine zamaliza duru ya tatu ya mazungumzo ya amani bila matokeo muhimu
2022-03-08 08:59:47| CRI

Russia na Ukraine zamaliza duru ya tatu ya mazungumzo ya amani bila matokeo muhimu_fororder_VCG111372223448

Wajumbe wa Russia na Ukraine wameshindwa kufikia matokeo muhimu katika duru ya tatu ya mazungumzo ya amani yaliyofanyika nchini Belarus.

Baada ya mazungumzo, mkuu wa ujumbe wa Russia na msaidizi wa rais wa Russia Bw. Vladimir Medinsky, amesema mazungumzo kuhusu mambo ya kisiasa na kijeshi yanaendelea, lakini ni magumu sana, na ni mapema kuzungumza kuhusu mambo chanya.

Amesema wajumbe wa Russia wamepeleka nyaraka nyingi ikiwemo makubaliano, lakini upande wa Ukraine haujaweza kusaini moja kwa moja, na uliondoka na nyaraka hizo ili kuzipitia kwanza.

Pia amesema matarajio yao kuhusu mazungumzo hayajafikiwa, lakini wanatumai katika duru ijayo watapiga hatua zaidi. Mazungumzo hayo yalifanyika kwa saa tatu huko Belovezhskaya Pushcha katika mpaka kati ya Belarus na Poland.

Ameongeza kuwa pande mbili zimetatua suala la kuwahamisha raia wa kawaida, huku upande wa Ukraine ukiihakikishia Russia kuwa njia ya kibinadamu itafunguliwa jumanne wiki hii.