Kenya na Zimbabwe zasaini makubaliano ya kukuza uhusiano
2022-03-10 09:04:57| CRI

Serikali za Kenya na Zimbabwe zimesaini makubaliano saba yanayolenga kuimarisha uhusiano kati ya nchi hizo mbili.

Makubaliano hayo ambayo yote ni Hati za Maelewano (MoU) kuhusu mashauriano ya kisiasa na kidiplomasia, utalii na uhifadhi wa wanyamapori, na uchunguzi wa ajali za ndege za kiraia na ajali mbaya, yalisainiwa mjini Nairobi katika ziara ya siku tatu ya rais Emmerson Mnangagwa wa Zimbabwe nchini Kenya.

Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya amesema makubaliano hayo yataziwezesha Kenya na Zimbabwe kushirikiana katika kutatua changamoto zinazozikabili, hasa suala la vijana kukosa ajira.

Rais Kenyatta pia ametoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuondoa vikwazo dhidi ya Zimbabwe, akivitaja kuwa ni haramu na visivyo vya haki.