Mawaziri wa mambo ya nje wa Russia na Ukraine wasema wako tayari kuendelea na mazungumzo kuhusu mgogoro
2022-03-11 08:56:39| CRI

Waziri wa mambo ya nje wa Russia Bw. Sergei Lavrov na mwenzake wa Ukraine Bw. Dmytro Kuleba jana walikutana na kufanya mazungumzo mjini Antalya, Uturuki, kwa uenyeji wa mwenzao wa Uturuki Mevlut Cavusoglu, lakini hawakupata maendeleo yoyote kuhusu kusimamisha mapambano. Huu ulikuwa ni mkutano wa kwanza wa ngazi ya juu kati ya pande hizo mbili tangu mgogoro uanze.

Baada ya mkutano wao Bw. Kuleba aliwambia wanahabari kuwa yuko tayari kuendelea kukutana na Bw. Lavron kwa utaratibu kama huo wa upatanishi wa Uturuki, na Bw. Lavrov amesema anapenda kuendelea na mazungumzo hayo kwa utaratibu huu lakini nchini Belarus. Amesema mkutano wao wa Antalya hauna lengo la kubadili mazungumzo yanayoendelea Belarus, lakini kama unaweza kusaidia unaweza kufanyika kwa utaratibu mwingine.

Uturuki imesema iko tayari kuendelea na juhudi za kidiplomasia kati ya Russia na Ukraine, na imefanya kazi ya mpatanishi na pande mbili hazijapinga kukutana katika siku za baadaye.