Chama tawala nchini Ethiopia chamaliza mkutano wa kwanza na kuahidi kukabiliana na mgogoro uliopo
2022-03-15 08:51:49| CRI

Chama tawala cha Ustawi cha nchini Ethiopia (PP) kimemchagua Waziri Mkuu Abiy Ahmed kuwa mwenyekiti wake katika mkutano uliojadili kuongezeka kwa hali ya wasiwasi katika jamii, uchumi na siasa nchini humo.

Chama hicho ambacho kilifanya mkutano wake wa kwanza kuanzia tarehe 11 hadi 13 mwezi huu, kimesema kimefikia maafikiano kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu hali ya sasa ya nchi hiyo na mwelekeo wa siku zijazo.

Pia mkutano huo umemteua naibu Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Demeke Mekonnen na Adem Farah, ambaye ni mkuu wa Ofisi ya Chama, kuwa makamu wenyeviti wa chama.

Mkutano huo umefanyika wakati nchi hiyo ikikabiliwa na mgogoro uliodumu kwa mwaka mmoja katika eneo la kaskazini, ukame katika sehemu za kusini mashariki mwa nchi hiyo, na hali mbaya ya kiuchumi na kuongezeka kwa chuki za kikabila.