Ofisa mwandamizi wa China afafanua msimamo wa China kuhusu suala la Ukraine
2022-03-15 10:42:32| cri

Mjumbe wa Ofisi ya Siasa ya Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China (CPC) Bw. Yang Jiechi jana Jumatatu alifafanua msimamo wa China kuhusu suala la Ukraine alipokutana na mshauri wa usalama wa taifa wa Marekani Bw. Jake Sullivan huko Rome.

Bw. Yang, ambaye pia ni mkurugenzi wa Ofisi ya Kamisheni ya Mambo ya Nje ya Kamati Kuu ya CPC, alisema kuwa upande wa China hautaki kuona hali ya Ukraine inafikia hatua ya sasa.

Amesema, China siku zote inasisitiza kuheshimu mamlaka na ukamilifu wa ardhi wa nchi zote, na kufuata kwa makini Katiba ya Umoja wa Mataifa, akiongeza kuwa China inajitahidi kuhimiza mazungumzo ya amani.

Bw. Yang ametoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuunga mkono kwa pamoja mazungumzo ya amani kati ya Russia na Ukraine, ili matokeo halisi yaweze kupatikana haraka iwezekanavyo, na mvutano uweze kupunguzwa mapema iwezekanavyo.

Bw. Yang pia amesisitiza kuwa China inapinga kauli au vitendo vyovyote vya kueneza taarifa potofu kuhusu msimamo wa China.