Kenya yaimarisha hatua za kukabiliana na ukame
2022-03-16 08:31:52| CRI

Msemaji wa serikali ya Kenya Bw. Cyrus Oguna jana amesema, serikali hiyo imeongeza usambazaji wa msaada wa dharura wa chakula, uhamishaji wa pesa na usafirishaji wa maji katika kaunti zilizoathiriwa na ukame ili kuepusha janga la kibinadamu.

Bw. Oguna amesema hatua zinazoendelea za kukabiliana na ukame zinalenga takriban wananchi milioni 2.8 katika kaunti 23 kame na nusu kame, ambao wamekosa mavuno na kutatizika kwa maisha kutokana na ukosefu wa mvua.

Bw. Oguna amesema, ili kupunguza mateso ya watu walioathiriwa na ukame, serikali imeanzisha hatua ambazo ni pamoja na uhamishaji wa pesa za dharura, usambazaji wa chakula na usafirishaji wa maji kwa malori ili kuhudumia mifugo na matumizi ya nyumbani.