Shughuli za walemavu zapata maendeleo nchini China
2022-03-16 12:37:22| cri

Shughuli za walemavu zapata maendeleo nchini China_fororder_273274_800x20000

Michezo ya Olimpiki ya Walemavu ya Majira ya Baridi ya Beijing imefungwa tarehe 13 Machi. Kama kioo, michezo hiyo haioneshi tu moyo wa kujiendeleza wa walemavu, lakini pia inaonyesha mafanikio ya shughuli za walemavu nchini China.

Katika Michezo hiyo, wanariadha wa China walishinda medali 18 za dhahabu, medali 20 za fedha na medali 23 za shaba, na kushika nafasi ya kwanza katika orodha ya medali.

Nje ya uwanja wa michezo, watu wengine wenye ulemavu wanafurahia michezo. Kiwango cha walemavu kushiriki kwenye mambo ya kitamaduni na michezo kimeendelea kuongezeka kutoka asilimia 6.8 mwaka 2015 hadi asilimia 23.9 mwaka 2021. Katika shule na vyuo, wanafunzi wenye ulemavu wameshiriki sana katika michezo mbalimbali. Idadi ya walemavu wanaoshiriki moja kwa moja kwenye michezo ya theluji na barafu imeongezeka kutoka watu 10,000 hadi zaidi ya watu 300,000.

Kuna walemavu milioni 85 nchini China, na shughuli za maendeleo ya walemavu zinatiliwa maanani sana. Rais Xi Jinping wa China aliwahi kusisitiza kwamba watu wenye ulemavu ni kundi lenye matatizo maalum, na wanahitaji ufuatiliaji na masaada zaidi. Ili kuboresha maisha ya walemavu na kukuza maendeleo yao, China imechukua hatua na sera mbalimbali. Hasa tangu kufanyika kwa Mkutano wa 18  wa Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China, shughuli za maendeleo ya walemavu zimepiga hatua kwa haraka.

Kukuza ajira ni njia muhimu ya kuwasaidia watu wenye ulemavu kujiunga na jamii na kutimiza ndoto zao za maisha. China imetekeleza sera mbalimbali za kipaumbele katika kuhimiza ajira ya walemavu, kama vile kuwapangia kazi, kuanzisha viwanda maalum vya walemavu, na kuwasaidia kuwa wajasiriamali. Katika kipindi cha Mpango wa 13 wa Maendeleo ya Miaka Mitano, walemavu milioni 1.81 walipata ajira mijini na vijijini, na wastani wa walemavu 400,000 walishiriki katika mafunzo ya ufundi stadi yanayofadhiliwa na serikali kila mwaka.

Nchini China kuna aina mbili za ruzuku, ambazo ni “Ruzuku ya Kuishi kwa Walemavu wenye Matatizo ya kiuchumi” na “ Ruzuku ya Utunzaji kwa Watu wenye Ulemavu Mbaya”. Katika kipindi cha Mpango wa 13 wa Maendeleo ya Miaka Mitano, ruzuku hizo ziliwanufaisha zaidi ya walemavu maskini milioni 12 na zaidi ya watu milioni 14 wenye ulemavu mbaya. Katika kipindi cha Mpango wa 14 wa Maendeleo ya Miaka Mitano, walemavu wote husika watanufaika na ruzuku hizo.

China pia imechukua hatua mbalimbali kuboresha kiwango cha elimu cha walemavu. Katika kipindi cha Mpango wa 13 wa maendeleo ya Miaka Mitano, jumla ya watu 57,477 wenye ulemavu walijiunga na vyuo vikuu, ambalo ni ongezeko la asilimia 50.11 ikilinganishwa na kipindi cha Mpango wa 12 wa Maendeleo ya Miaka Mitano.

Ili kukuza ushiriki wa walemavu katika michezo, China ilitoa waraka kuhusu Maendeleo ya Michezo kwa Walemavu. Kupitia kushiriki katika michezo, walemavu wanaweza kuongeza mawasiliano ya kijamii, kujifurahisha na kujiamini zaidi.

Michezo ya Olimpiki ya Walemavu ya Majira ya Baridi ya Beijing imefungwa, lakini maendeleo ya walemavu nchini China yanazidi kupamba moto. Katika zama mpya, maisha ya walemavu nchini China hakika yatakuwa bora zaidi.