China yasisitiza kukabiliana na janga la COVID-19 kwa njia bora na kali zaidi
2022-03-18 13:53:38| Cri

Kamati ya Kudumu ya Ofisi ya Siasa ya Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China (CPC) iliitisha mkutano jana Alhamisi kuangalia hali ya janga la COVID-19 na kupanga njia bora na kali zaidi katika kukabiliana nalo. Katibu mkuu wa Kamati Kuu ya CPC Xi Jinping aliongoza mkutano huo na kutoa hotuba muhimu.

 

Xi alisema tangu kupitishwa kwa hatua za kawaida za kuzuia na kudhibiti janga hilo, China imedumisha sera ya "kuzuia maambukizi yanayotoka nje na kuibuka tena ndani ya nchi". Xi alisema mbinu za aina tofauti za kuzuia na kudhibiti janga zimeboreshwa kulingana na hali ya mikoa na viwango tofauti vya kuibuka tena mara kwa mara, na kwa sababu hiyo, maambukizi yaliyotokea katika maeneo kadhaa yamedhibitiwa haraka na afya na usalama wa watu umelindwa kwa kiwango kikubwa zaidi, jambo ambalo limeonyesha nguvu na uwezo thabiti wa nchi katika kuzuia na kudhibiti janga hili na nguvu ya uongozi wa Chama cha Kikomunisti cha China na mfumo wa ujamaa wa China.

 

Xi alisisitiza kuwa ushindi unatokana na ustahimilivu. Mamlaka zote za mitaa na idara za serikali lazima zifahamu kikamilifu kazi zenye utata, ugumu na za kudumu za kudhibiti COVID-19 ndani na nje ya nchi, kuhamasisha zaidi jamii nzima, kujenga maelewano, kuendelea na kazi kwa ujasiri mkubwa na uvumilivu, na pia kwa njia thabiti na ya uangalifu zaidi. Aliwahimiza kutoa kipaumbile kwa watu na maisha yao, kuzingatia mbinu madhubuti ya kuondoa kabisa maambukizi kwa mujibu wa sayansi na hatua zinazolengwa, na kudhibiti kuenea kwa ugonjwa huo haraka iwezekanavyo. Amesisitiza kuongeza utafiti na utengenezaji wa chanjo, vitendanishi vya upimaji wa haraka na dawa ili kudhibiti janga hili. Xi pia alitoa wito wa kudumisha mwelekeo wa kimkakati, kutafuta maendeleo wakati wa kuhakikisha utulivu, kuratibu mwitikio wa COVID-19 na maendeleo ya kiuchumi na kijamii, , kuchukua hatua madhubuti zaidi, kujitahidi kufikia matokeo mazuri kwa gharama ndogo zaidi, na kupunguza athari za janga hili kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii.