Bidhaa nyingi zaidi za kilimo za Afrika kuingia katika soko la China
2022-03-21 14:13:52| CRI

Bidhaa nyingi zaidi za kilimo za Afrika kuingia katika soko la China_fororder_农产品

Ripoti iliyotolewa hivi karibuni na gazeti la the South China Morning Post imesema hatua ya mamlaka za forodha za China kurahisishia utaratibu wa biashara na baadhi ya nchi za Afrika imeruhusu bidhaa nyingi zaidi za kilimo kutoka bara hilo kuingia China.

Ripoti hiyo inasema Afrika Kusini, Kenya na Zimbabwe ni miongoni mwa nchi za Afŕika ambazo hivi majuzi zimetia saini utaratibu uliorekebishwa wa kuziruhusu kufikia soko la China.

Mwezi uliopita, Afrika Kusini ilisafirisha shehena yake ya kwanza ya malimau 100,000 hadi China. Mwezi Desemba pia ilitia saini utaratibu mpya na China juu ya mauzo ya nje ya mapea, ambapo inatarajiwa kuongeza asilimia 22 ya mauzo ya mapea nje ya nchi hiyo kwenda Mashariki ya Mbali.

Tanzania ilianza kuuza soya nchini China mwaka 2020. Mikataba kama hiyo imesainiwa kwa maparachichi, chai, kahawa na mawaridi kutoka Kenya, kahawa na soya kutoka Ethiopia, bidhaa za nyama kutoka Namibia na Botswana, matunda kutoka Afrika Kusini na kahawa kutoka Rwanda.

Kampuni ya kimataifa ya utafiti na ushauri ya Oxford Business Group ilibainisha katika ripoti yake ya hivi majuzi kwamba licha ya changamoto za usambazaji wa kimataifa, biashara kati ya China na Afrika ilipanda hadi kufikia viwango vya juu mwaka 2021.