Msomi wa Mali: Mikutano Miwili ya China yatoa ishara ya amani duniani
2022-03-22 08:16:46| CRI

Msomi wa Mali: Mikutano Miwili ya China yatoa ishara ya amani duniani_fororder_Yoro

Wakati mgogoro kati ya Russia na Ukraine unazidi kupamba moto, Mikutano Miwili ya China, ambayo ni Mkutano wa tano wa Baraza la 13 la Mashauriano ya Kisiasa la China na Mkutano wa tano wa Bunge la 13 la Umma la China, imekuwa dirisha muhimu kwa dunia ya nje kufuatilia mwelekeo wa diplomasia ya China. Aliyekuwa mwanadiplomasia wa Mali na mtaalamu wa masuala ya kimataifa Prof. Yoro Diallo hivi karibuni amesema, China ikiwa ni mjenzi wa amani ya dunia, mchangiaji wa maendeleo ya dunia na mlinzi wa utaratibu wa kimataifa, Mikutano Miwili ya China imetoa ishara ya amani kwa dunia nzima.

Profesa Diallo anaona kuwa Ripoti kuhusu Kazi ya Serikali ya mwaka huu imesisitiza kuwa China itasukuma mbele kufikiwa kwa makubaliano ya kiwango cha juu ya biashara huria kati yake na nchi na sehemu nyingi zaidi, mpango unaoonesha nia ya China ya kuimarisha ushirikiano wa kunufaishana na nchi mbalimbali duniani. Waziri wa mambo ya nje wa China Bw. Wang Yi alipokutana na wanahabari baada ya Mikutano Miwili kumalizika, alijibu maswali kuhusu suala la Ukraine, uhusiano kati ya China na Marekani na suala la “Ukanda Mmoja, Njia Moja”, ambapo alisisitiza mara nyingi msimamo wa China wa kupinga “vita mpya ya baridi”, na kuonesha uwajibikaji wa China katika kuendelea kusukuma mbele ujenzi wa Jumuiya ya Binadamu yenye Hatma ya Pamoja.

Prof. Diallo amefuatilia zaidi ishara za ushirikiano kati ya China na Afrika zilizotolewa kwenye Mikutano Miwili. Amesema, waziri wa mambo ya nje wa China hufanya ziara yake ya kwanza ya kila mwaka barani Afrika, desturi inayoonesha uungaji mkono thabiti wa China kwa maendeleo na ustawi wa Afrika. Katika miaka iliyopita, China imejenga reli yenye urefu zaidi ya kilomita elfu kumi, barabara zenye urefu zaidi ya kilomita laki moja, bandari karibu mia moja na idadi isiyohesabika ya hospitali na shule katika bara la Afrika. Matunda hayo ya ushirikiano yameboresha kwa kiasi kikubwa maisha ya watu wa Afrika na kuchochea maendeleo ya Afrika.  Amesema, mwaka huu ni wa kwanza kutekeleza matokeo yaliyopatikana kwenye mkutano wa nane wa mawaziri wa Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika FOCAC. Waziri wa mambo ya nje Bw. Wang Yi alisema kwenye mkutano na wanahabari kuwa, China itapiga jeki ushirikiano kati yake na Afrika kwenye mapambano dhidi ya janga la Corona, kuinua ubora na viwango vya ushirikiano halisi kati ya pande hizo mbili, na kusukuma mbele utekelezaji wa “Ruwaza ya Maendeleo ya Amani katika Pembe ya Afrika”, hatua ambazo Prof. Diallo anaona kuwa zimedhihirisha mara nyingine tena uaminifu na uwajibikaji wa China katika kutekeleza ahadi ilizotoa kwenye ushirikiano kwa Afrika.