Barabara iliyojengwa na China yapunguza msongamano wa magari Botswana
2022-03-23 10:43:11| CRI

Waziri wa uchukuzi na mawasiliano wa Botswana Thulaganyo Segokgo jana alipohudhuria hafla ya ufunguzi wa barabara kijijini Boatle, takriban kilomita 44 kutoka Gaborone amesema, barabara ya Gaborone-Boatle iliyojengwa na kampuni za China CSCEC na CCC imechangia kupunguza msongamano wa magari kati ya Gaborone na Lobatse.

Amesema barabara hiyo imesaidia kupunguza muda wa usafiri huko Greater Gaborone na sehemu nyingine zilizoko kwenye eneo hilo, pia imeboresha hali ya usafiri na kuongeza ufanisi wa uzalishaji wa sekta za kiuchumi.

Mradi huo wa ujenzi wa barabara uliogharimu takriban dola milioni 103 za kimarekani ulianza kutekelezwa mwaka 2017 na ulitarajiwa kumalizika mwaka 2019, lakini ulichelewa kutokana na uhaba wa vifaa tangu liibuke janga la Corona. Habari kutoka polisi ya Botswana imesema tangu barabara hiyo ijengwe ajali za barabarani zimepungua.