Baraza la Usalama lashindwa kupitisha azimio kuhusu hali ya kibinadamu nchini Ukraine
2022-03-24 10:56:41| CRI

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lenye wanachama 15 Jumatano lilishindwa kupitisha azimio kuhusu hali ya kibinadamu nchini Ukraine.

Wanachama wawili (Russia na China) walipiga kura kuunga mkono azimio hilo na wengine 13 hawakupiga kura. Azimio hilo lililowasilishwa na Russia lilikataliwa.

Azimio la Baraza la Usalama linahitaji angalau kura tisa za ndio na hakuna kura ya turufu kutoka kwa Russia, China, Uingereza, Ufaransa au Marekani ili kupitishwa.

Rasimu ya azimio la Russia inaonyesha wasiwasi mkubwa kuhusu ripoti za vifo vya raia na kuzorota kwa hali ya kibinadamu ndani na jirani na Ukraine, ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa idadi ya watu waliopoteza makazi na wakimbizi. Azimio hilo pia linataka ulinzi wa raia, wakiwemo wafanyakazi wa kibinadamu na matibabu, kuheshimiwa kwa mujibu wa sheria za kimataifa na ulinzi wa vitu vya kiraia na miundombinu muhimu, uhamishaji salama na bila vikwazo wa raia wote, na upatikanaji wa msaada wa kibinadamu bila vikwazo nchini Ukraine.

Baraza la Usalama limefanya mikutano mitatu kuhusu hali ya kibinadamu nchini Ukraine tangu mzozo huo ulipozuka, Februari 28, Machi 7 na Machi 17 mtawalia.