Viongozi wa Afrika waazimia kukabiliana na uhalifu wa mtandao wa internet na kuimarisha usalama wa kidijitali
2022-03-25 10:07:01| CRI

Mkutano wa siku mbili wa wakuu wa nchi na serikali wa Afrika juu ya Usalama kwenye mtandao wa internet umefungwa jana Alhamis, na kupitishwa azimio la Afrika kuhusu usalama wa mtandao wa internet na kupambana na uhalifu wa kimtandao katika Afrika.

Mkutano huo ulioandaliwa na Tume ya Uchumi ya Umoja wa Mataifa kwa Afrika (ECA) ikishirikiana na serikali ya Togo, ulilenga kutathimini hali ya usalama wa mtandao wa internet na kupendekeza sera kwa ajili ya serikali za Afrika.

Akiongea kwenye mkutano huo rais wa Togo, Faure Essozimna Gnassingbe, ameeleza umuhimu wa kuendeleza ushirikiano wa kupambana na uhalifu kwenye mfumo wa ikolojia wa kidijitali, ambayo ni mapinduzi ya wakati huu yanayofungua fursa kubwa kwa binadamu. Ametoa wito kwa viongozi wengine wa nchi za Afrika kutambua Mkataba wa Usalama wa Mtandao wa Internet na Ulinzi wa Taarifa Binafsi uliopitishwa huko Malabo, Guinea ya Ikweta Juni 2014, na kusema kwa kufanya hivyo kutazidisha ushirikiano kati ya nchi wanachama wa Umoja wa Afrika juu ya ulinzi wa taarifa binafsi na za nchi.