Peng Liyuan ahutubia kipindi cha mjadala cha WHO kwa njia ya video Siku ya Kifua Kikuu Duniani
2022-03-25 10:10:20| CRI

Peng Liyuan, mke wa Rais Xi Jinping wa China na balozi mwema wa Shirika la Afya Duniani (WHO) wa kifua kikuu TB na UKIMWI, siku ya Alhamisi alihutubia kipindi cha mjadala kwa njia ya video kilichoandaliwa na WHO ili kuadhimisha Siku ya Kifua Kikuu Duniani.

Peng alisema, katika miaka ya hivi karibuni, kutokana na juhudi kubwa za WHO na juhudi za pamoja za jumuiya ya kimataifa, dunia imepata mafanikio makubwa katika mapambano dhidi ya TB. Alisisitiza kuwa serikali ya China inazingatia sana kinga na matibabu ya TB, na imeiingiza katika mkakati wa Afya wa China. Fedha maalum zimetengwa, upimaji bila malipo na dawa za TB zinatolewa kwa wagonjwa, na kiwango cha uponaji kwa ugonjwa wa TB kimeendelea kuwa zaidi ya asilimia 90.

Peng aliongeza kuwa hata wakati wa janga la COVID-19, serikali ya China na sekta zote za jamii zimechukua hatua madhubuti kuwahudumia wagonjwa wa TB na kuhakikisha matibabu yao yanaendelea.

Peng alisema tangu aanze kushiriki katika juhudi za kupambana na TB muongo mmoja uliopita, ametembelea vituo vingi vya matibabu, shule na jamii, na kushuhudia mamilioni ya wafanyakazi wa matibabu na watu wa kujitolea wakihudumu kama walinzi wa afya, kwa upendo na vitendo.