Rais Xi Jinping wa China afanya mazungumzo kwa njia ya simu na Rais mteule wa Korea Kusini Yoon Suk-yeol
2022-03-25 19:24:52| cri

Rais Xi Jinping wa China leo ijumaa amefanya mazungumzo kwa njia ya simu na Rais mteule wa Korea Kusini Bw. Yoon Suk-yeol, na kumpongeza kwa mara nyingine tena kuchaguliwa kuwa rais wa Korea Kusini.

Rais Xi amefahamisha kuwa China na Korea Kusini ni majirani wa karibu wa kudumu, na pia ni washirika wasioweza kutenganishwa, na kuongeza kuwa China daima inatilia maanani uhusiano kati yake na Korea Kusini.

Amesema kutokana na juhudi za pamoja za pande mbili, uhusiano wa nchi hizo umeendelea kwa kasi katika nyanja zote, na kuwa washirika wa kimkakati. Ukweli umethibitisha kuwa maendeleo ya uhusiano kati ya China na Korea Kusini yanaendana na maslahi ya kimsingi ya nchi hizo mbili na watu wake, na kuhimiza amani na maendeleo ya kikanda.

Rais Xi pia amekumbusha kuwa huu ni mwaka wa 30 wa maadhimisho ya uhusiano wa kidiplomasia kati ya nchi hizo mbili, na pande hizi mbili zinapaswa kutumia fursa hii kuimarisha kuheshimiana, uaminifu wa kisiasa, urafiki kati ya watu wa nchi zao na kusukuma mbele maendeleo ya kudumu na ya muda mrefu ya uhusiano kati ya China na Korea Kusini.

Rais Xi pia amezungumzia hali ya kimataifa, akisema kwa sasa jumuiya ya kimataifa inakabiliwa na changamoto nyingi, China na Korea Kusini zina wajibu wa kudumisha amani ya kikanda na kuhimiza ustawi wa dunia. Amesisitiza kuwa China iko tayari kushirikiana na Korea Kusini kuimarisha ushirikiano wa kimataifa na kikanda, na kufanya juhudi za dhati ili kuhakikisha utulivu na mwendelezo wa minyororo ya kimataifa ya viwanda na usambazaji.