Uganda yawataka wananchi watulie wakati misukosuko ilisababisha mfumuko wa bei nchini humo
2022-03-28 08:47:58| CRI

Wizara ya fedha ya Uganda imesema misukosuko kadhaa ya kimataifa imefanya bei ya bidhaa nchini Uganda ipande na kuleta usumbufu kwa watu.

Waziri wa fedha wa Uganda Bw. Matia Kasaija amesema kwenye taarifa ya hivi karibuni kuwa bei ya bidhaa za msingi kama vile sabuni za kufulia, unga wa ngano, mafuta ya kupikia, vifaa vya shule na gharama za usafiri, zimepanda kutokana na msukosuko wa Ukraine na janga la COVID-19.

Amesema mbali na changamoto hizo mbili, katika siku za hivi karibuni uchumi wa dunia pia ulitatizwa na gharama kubwa za usafirishaji wa mizigo kwa njia ya meli, kukosekana kwa makontena ya kusafirishia mizigo na kupanda kwa gharama za usafirishaji, kulikosababisha upungufu wa upatikanaji wa bidhaa duniani. Lakini pia kufunguliwa kwa uchumi duniani kufuatia kudhibitiwa kwa janga la COVID-19 kumefanya bei za bidhaa zipande kutokana na kuongezeka kwa mahitaji.