UM wapata miili ya watu wanane waliokuwa kwenye helikopta ya walinzi wa amani iliyoanguka DRC
2022-03-30 08:53:39| CRI

Ofisi ya habari ya Umoja wa Mataifa imesema miili minane ya watu waliokuwa kwenye helikopta ya Umoja wa Mataifa iliyoanguka jana Kivu Kaskazini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imepatikana.

Helikopta ya ukubwa wa kati aina ya Puma ilikuwa inafanya operesheni ya kufuatilia usalama kwa ajili ya tume ya ulinzi wa amani ya Umoja wa Mataifa nchini humo MONUSCO.

Ndege hiyo ilikuwa ikifanya operesheni hiyo kwenye eneo lililokumbwa na mapigano kati ya wapiganaji wa kundi la M23 na jeshi la serikali. Jeshi la serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo limesema helikopta hiyo ilitunguliwa na waasi wa kundi la M23, lakini Umoja wa Mataifa bado haujathibitisha madai hayo.