Siku ya Afya Duniani: Ugonjwa wa Endometriosis
2022-04-08 08:30:55| Cri

Kila ifikapo Aprili 7, ni Siku ya Afya Duniani ambapo Shirika la Afya Duniani (WHO) huamua kuangazia mada maalum katika ulimwengu wa afya na matibabu. Kuanzia kwenye afya ya akili hadi bima na kila kitu kinachohusiana na hayo, siku hii hupaza sauti ya kile kitakachojadiliwa duniani. Siku ya Afya Duniani ya mwaka huu imeangazia wauguzi na wakunga, wafanyakazi wa huduma ya simu na wafanyakazi wasiotulia ambao wameleta mapinduzi makubwa katika tasnia ya afya.

Je, tunaweza kufikiria upya ulimwengu ambao hewa safi, maji na chakula vinapatikana kwa wote? Ambao uchumi unazingatia afya na ustawi? Na ambao miji inaweza kukalika na watu wana udhibiti wa afya zao na afya ya sayari? Haya ndio maswali yanayozunguka kwenye vichwa vya watu na kupelekea kuibuliwa kwa kauli mbiu ambayo ni “Sayari yetu, Afya zetu".

Tukiwa tupo katikati ya janga la COVID-19, sayari iliyochafuliwa, kuongezeka kwa magonjwa kama vile saratani, pumu, ugonjwa wa moyo na mengineyo, Siku ya Afya Duniani ya mwaka huu wa 2022, WHO itajikita zaidi kwenye hatua za haraka zinazohitajika kuwafanya binadamu wawe na afya na sayari yenye afya na kukuza harakati za kuunda jamii zinazozingatia ustawi.

WHO inakadiria kuwa zaidi ya vifo milioni 13 kote duniani kila mwaka vinatokana na sababu zinazoweza kuepukika. Hii ni pamoja na msukosuko wa hali ya hewa ambao ndio tishio kubwa zaidi la kiafya linalowakabili binadamu. Msukosuko wa hali ya hewa pia ni shida ya kiafya. Hivyo katika kuadhimimisha siku hii ya afya duniani, ingawa tayari imeshapita lakini leo kwenye Ukumbi wa Wanawake tumeona ni vyema tukagusia tatizo ambalo linawasumbua zaidi kina dada na wanawake. Ugonjwa wa Endometriosis unaowapata wanawake wakifikia katika siku zao za hedhi.