Waziri wa mambo ya Nje ya China afanya mazungumzo na mwenzake wa Ukraine
2022-04-05 08:42:01| CRI

Waziri wa Mambo ya Nje ya China Bw. Wang Yi jana alifanya mazungumzo kwa njia ya simu na mwenzake wa Ukraine Dmytro Kuleba kuhusu hali ya Ukraine.

Bw. Wang aliipongeza serikali ya Ukraine kwa juhudi zake za kuhakikisha usalama wa raia wa China walioondoka Ukraine, na kusema anatumai Ukraine itaendelea kuchukua hatua madhubuti ili kuhakikisha usalama wa raia wachache wa China ambao wamebaki nchini humo.

Pia amesema, msimamo wa kimsingi wa China kuhusu suala la Ukraine ni kuhimiza amani na mazungumzo, na China inapenda kushikilia msimamo wake na kuendelea kutoa mchango katika utatuzi wa suala hilo.

Kwa upande wake, Bw. Kuleba amesema Ukraine inatilia maanani sana ushawishi na heshima ya China katika mambo ya kimataifa, na kuongeza kuwa, nchi yake iko tayari kudumisha mawasiliano na China, na kutarajia China kuendelea kuchukua nafasi muhimu katika kusimamisha vita.