Viongozi wa Somalia watakiwa kukumbatia maafikiano ili kukamilisha mchakato wa uchaguzi
2022-04-06 08:47:32| CRI

Wenzi wa kimataifa wa Somalia wamewataka viongozi wa nchi hiyo kukumbatia mazungumzo na maafikiano katika hatua ya mwisho ya kukamilisha mchakato wa uchaguzi.

Katika taarifa yao ya pamoja iliyotolewa jana mjini Mogadishu, wenzi hao, ikiwa ni pamoja na nchi za Magharibi na Umoja wa Afrika, Umoja wa Ulaya na Umoja wa Mataifa, wamesema zaidi ya asilimia 91 ya wabunge wamechaguliwa, hivyo inapaswa kuhakikisha kasi hiyo inatumika kumalizia viti vilivyobaki vya bunge hilo.

Wenzi hao wamewataka viongozi kutoa kipaumbele kwa umuhimu wa majadiliano na mawasiliano ili kukamilisha mipango ya uchaguzi, hususan katika mkoa wa Jubaland, ili kuhakikisha jamii husika zinawakilishwa katika bunge lijalo.

Hata hivyo, wenzi hao wamesikitishwa na ukiukaji wa sheria za uchaguzi nchini humo na kushindwa kutimia kwa asilimia 30 ya wawakilishi wanawake katika bunge kama ilivyoelekezwa katika makubaliano yaliyofikiwa Septemba 17, 2020.