Uganda na Kenya zasaini makubaliano ya ushirikiano wa ulinzi na usalama
2022-04-08 08:30:10| CRI

Wizara ya ulinzi ya Uganda imesema, nchi hiyo na Kenya zimesaini makubaliano kuhusu ulinzi na usalama, ambayo yatahimiza ushirikiano wa kukabiliana na matishio kama vile ugaidi.

Makubaliano hayo yamesainiwa na waziri wa ulinzi wa Uganda Vincent Ssempijja na mwenzake wa Kenya Eugene Wamalwa.

Bw. Ssempijja amesema, kuna haja ya kupambana na uhalifu wa kuvuka mipaka ikiwemo ugaidi na usambazaji wa silaha ndogo. Pia ameipongeza Kenya kwa ushirikiano katika kufufua makubaliano ya ushirikiano katika ulinzi na usalama kati ya nchi hizo mbili.

Kwa upande wake, Bw. Wamalwa amesema, baada ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kujiunga na Jumuiya ya Afrika Mashariki, upanuzi huo unakuja na changamoto, hasa ugaidi. Ameishukuru Uganda kwa kusaidia kutuliza hali katika eneo la mashariki ya DRC na kutaka ushirikiano huo kuimarishwa katika ulinzi na usalama.