EAC yawakumbuka watu zaidi ya milioni moja waliouawa katika Mauaji ya Kimbari nchini Rwanda mwaka 1994
2022-04-08 08:46:02| CRI

Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) jana iliadhimisha kumbukizi ya miaka 28 ya mauaji ya kimbari yaliyotokea nchini Rwanda kwa kuweka mashada ya maua kama heshima kwa watu zaidi ya milioni moja waliouawa katika mauaji hayo.

Taarifa iliyotolewa katika makao makuu ya Jumuiya hiyo mjini Arusha, Tanzania imesema, shughuli hiyo iliwakutanisha wadau wa ngazi mbalimbali, wakiwemo wawakilishi kutoka dini mbalimbali, Baraza la Biashara la Afrika Mashariki, na wafanyakazi wa Jumuiya hiyo.

Akizungumza kwenye hafla hiyo, Katibu Mkuu wa EAC Peter Mathuki amerejea tena ahadi ya sekretariet ya jumuiya hiyo kuwa, Jumuiya ya Afrika Mashariki itaendelea kuhakikisha kuwa hisia za mauaji ya kimbari zinaondolewa katika kanda hiyo kupitia majadiliano na tathmini za hatari za nadharia za mauaji ya kimbari.