UM, AU na IGAD watoa wito wa kufanyika mazungumzo ya kumaliza mzozo wa kisiasa nchini Sudan
2022-04-13 09:08:45| cri

Vyombo vya Kimataifa vikiwemo Umoja wa Mataifa (UM), Umoja wa Afrika (AU) na Shirika la Maendeleo la Serikali za Nchi za Afrika Mashariki (IGAD) jana vimeitaka serikali ya Sudan kutumia mbinu za kujenga mazingira yanayofaa kwa ajili ya mazungumzo ya kumaliza mzozo wa kisiasa nchini humo.

Wito huo umetolewa wakati mwenyekiti wa Baraza la Mpito la Utawala wa Sudan Abdel Fattah Al-Burhan alipopokea ujumbe unaotoka kwenye vyombo hivyo vitatu, akiwemo mkuu wa Tume ya Umoja wa Mataifa nchini Sudan Volker Perthes, mjumbe maalumu wa AU nchini Sudan Mohamed El Hacen Ould Lebatt na mwakilishi wa IGAD Ismail Wais.

Mohamed Belaish, msemaji wa vyombo hivyo vitatu, amenukuliwa kwenye taarifa yake akisema, vyombo hivyo kupitia juhudi zake, vinataka kujenga maelewano ya kisiasa kulingana na makubaliano mapana zaidi miongoni mwa Wasudan.